Na: Maiko Luoga GEITA.

Maaskofu wa Kanisa Anglikana mei 19 mwaka huu wakiongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa, wamefika Wilayani Chato mkoani Geita na kutembelea kaburi la aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt, John Pombe Magufuli.

Akizungumza mara baada ya kuwasili mahali alipozikwa hayati Magufuli Wilayani Chato na kufanya Ibada maalumu ya shukrani na kukumbuka maisha yake, Mhashamu Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa amesema Hayati Magufuli ataendelea kukumbukwa kwa alama za maendeleo alizoziacha katika maeneo tofauti nchini.

“Kanisa Anglikana Tanzania tukiwakilishwa na Maaskofu wetu kutoka maeneo tofauti ya nchi tumefika hapa Chato kwa lengo la kufanya ibada ya shukrani na kumbukumbu ya maisha ya Hayati Dkt, John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wetu ambae sasa hatunae tena” amesema Askofu, Dkt, Mndolwa.

Aidha amesema Serikali bado ina jukumu kubwa la kuyaishi mema yaliyoanzishwa na Hayati Dkt, John Pombe Magufuli na kuyatimiza kwa manufaa mapana ya Taifa, na kuongeza kuwa Uongozi wa Kanisa Anglikana Tanzania utaendelea kumuombea Rais wa sasa Mhe, Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake.

Vithalis Yusuph Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Biharamulo na Jackson Sosteness Jackson wa Dayosisi ya Dar Es Laam wasema Watanzania wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuishi maisha ya Hayati Dkt, John Pombe Magufuli ambae enzi za uhai wake kila wakati alisisitiza kufanya kazi na kumuomba Mungu.

Askofu, Dkt, Dickson Chilongani Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania (DEAN) ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kuendelea kuyatunza mazingira yanayozunguka eneo alilozikwa Hayati Magufuli kwa kujenga jengo zuri huku akiwataka Watanzania kuacha kusambaza taarifa za upotoshaji mitandaoni.

Kwa upande wake Bw, Gorodian Joseph Magufuli, Mdogo wa Hayati Dkt, John Pombe Magufuli, kwa niaba ya familia ameushukuru Uongozi wa Kanisa Anglikana Tanzania kwa kufika Wilayani Chato kuwafariji na kufanya ibada maalumu ya kuombea Roho ya mpendwa wao hayati Dkt, John Pombe Magufuli na familia yake.

Akizungumza na Maaskofu hao baada ya kuwasili Ofisini kwake wakitaka kujua kama miradi iliyoanzishwa na Hayati Magufuli Wilayani Chato Inaendelezwa, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe, Charles Kabeho alisema miradi hiyo inaendelea kutekelezwa na Serikali ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Geita uliopo Chato ambao umeanza kutumika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *